Sunday, 27 November 2016

PENZI MUTWLABU

Aaa, nilisemee penzi, lilojaa matamu ya ajabu
Tulilianza utoto ule, ujana mpaka sasa ubabu
Tukipeana visambusa, kashata pia kababu

Penzi letu mi na yule, mzuri wangu mahabubu
Hakika si msukule, bali ni penzi mutwlabu.

Mrembo kwa umbile, tabia ni mtaratibu
Nayapata ya maumbile, moyo hauna tabu
Ananipa jicho laini, kwa mtazamo wa aibu
Hakodoi kodo, hila ya moyo hitomsibu
Hakika si msukule, bali ni penzi mutwlabu.

Anayajua makao, ya bara, pwani na uarabu
Anahila za mwambao, kuni haishi kujibu
Anayafanya awezayo, bwana asimuharibu
Hii si nyama yao, na wala siipi lakabu
Hakika si msukule, bali ni penzi mutwlabu.

Mapishi alipojifunzia, hakika amerutubu
Anajua pangilia, vyakula kuviratibu
Si dagaa si bamia, katu hatoharibu
Jiko likimchezea, kwa ulimi ataratibu
Hakika si msukule, bali ni penzi mutwlabu.

Salamu kusalimia, kamwe haimpi tabu
Heshima ataitoa, kwa watoto, vijana, pia mababu
Yake asipopewa, kwa dua humjibu
Chuki ameikimbia, dhamana yake wahhabu
Hakika si msukule, bali ni penzi mutwlabu.

Ninamengi yakusemea, juu ya wangu muhibbu
Sifaze zilivyotulia, hakika si za aibu
Mipaka kuzingatia, hilo sitoharibu
Nisipoanglia, wabaya nitawakaribu
Hakika si msukule, bali ni penzi mutwlabu.

Tamati nimefikia, japo hayajesha
Jina nitawatajia, muweze jisongesha
Ni binti mwananjia, jinale furahisha
Hapo nimezamia, nayasogeza maisha
Mtu akituvamia, wallahi namuharibu
Hakika si msukule, bali ni penzi mutwlabu.

No comments:

Post a Comment